Mimbar ni nini?
Mimbar ni jukwaa la kupakia masomo ya Kiislamu — khutba, darsa, tafsiri — kwenye YouTube, na kuyaweka mahali pamoja ambapo wasikilizaji wanaweza kuyapata kwa urahisi.
Ni kwa ajili ya Masheikh na Misikiti. Wewe unapakia faili la sauti au video na kuandika kichwa; Mimbar inatengeneza picha ya jalada, inabadilisha sauti kuwa video ikihitajika, na inapakia somo kwenye chaneli YAKO ya YouTube.
Somo halikai Mimbar. Video huishi kwenye chaneli yako ya YouTube — Mimbar inaonyesha tu kiungo chake na kulipanga pamoja na masomo ya Masheikh na Misikiti mingine.
Mimbar imedhaminiwa na UKUEM (ukuem.org) na kutengenezwa na Himma Technologies.
Kupakia ni bure. Hakuna kikomo cha masomo kwa kawaida. Michango huisaidia Mimbar kuendelea kuwepo, lakini haununui chochote — soma sehemu ya "Mipaka na michango".
Unahitaji nini kabla ya kuanza?
- Akaunti ya Mimbar — ya msikiti au ya sheikh binafsi. Ni bure.
- Chaneli ya YouTube inayomilikiwa na wewe au msikiti wako. Kama huna, tengeneza moja kwenye youtube.com kwa akaunti ya Google.
- Faili la somo: sauti (MP3, M4A, WAV — hadi 500MB) au video (MP4, MOV, AVI — hadi 4GB).
- Ukitaka picha ya sheikh kwenye jalada: picha yake moja, ya wazi. Kama hutaki picha ya mtu kabisa, kuna njia tano zisizo na picha ya mtu — soma "Chagua picha ya jalada".
Somo refu kuliko dakika 15? Chaneli yako ya YouTube lazima iwe imethibitishwa kwa namba ya simu. Bila hivyo YouTube hukataa video ndefu — na hukataa BAADA ya kupakia kuisha. Thibitisha sasa kwenye youtube.com/verify; huchukua dakika mbili.
Hatua 1
Jisajili
Fungua ukurasa wa "Jisajili" na uchague aina ya akaunti:
- Msikiti — masomo yote ya msikiti kwenye chaneli moja. Utaandika jina la msikiti na jina la msimamizi. Kila somo linaweza kuwa na mzungumzaji tofauti.
- Sheikh binafsi — chaneli yako mwenyewe, jina lako kwenye kila somo. Utachagua cheo chako: Sheikh, Ustadh, Imam au Mwalimu.
Weka jina, barua pepe na nywila. Nywila iwe angalau herufi 8 na isiwe na jina lako ndani yake — ukurasa unakuonyesha ubora wa nywila unapoandika.
Baada ya kujisajili, msimamizi wa Mimbar anakagua akaunti yako kabla hujaweza kuchapisha. Hii ni ili masomo yachapishwe na Masheikh na Misikiti halali tu. Ukisubiri, unaweza kuingia, kuunganisha chaneli yako ya YouTube na kukamilisha wasifu wako. Utapata barua pepe ikishakubaliwa. Ukiona ujumbe "Akaunti yako inasubiri ukaguzi" — hakuna unachotakiwa kufanya; subiri tu.
Hatua 2
Unganisha chaneli yako ya YouTube
Mimbar haihifadhi video. Ili ipakie somo, inahitaji ruhusa ya kupakia kwenye chaneli yako. Nenda Mipangilio → "Chaneli ya YouTube" → "Unganisha YouTube". Utaelekezwa Google; chagua akaunti inayomiliki chaneli, kisha ukubali.
Ruhusa unayotoa ni ya chaneli yako ya YouTube pekee — si ya Gmail, si ya Drive, si ya kitu kingine cha Google. Mimbar inaitumia kwa mambo haya tu:
- Kupakia video za masomo unayoweka, na kuziwekea kichwa, maelezo, picha ya jalada na ratiba uliyochagua.
- Kusoma jina la chaneli na kama imethibitishwa, ili ikuonye kabla ya kupakia somo refu.
- Kusoma idadi ya watazamaji wa masomo ILIYOPAKIA yenyewe, ili kuonyesha kwenye dashibodi yako.
Mimbar haisomi maoni, wafuasi, wala video ambazo haikupakia. Haipakii chochote bila wewe kubonyeza "Thibitisha na anza uchapishaji".
Kinachohifadhiwa: kitambulisho na jina la chaneli, na ufunguo wa ruhusa (unaotunzwa kwa siri) unaoiruhusu Mimbar kupakia kwa niaba yako.
Unaweza kuondoa ruhusa wakati wowote: Mipangilio → Chaneli ya YouTube → "Tenganisha chaneli". Au kutoka akaunti yako ya Google: myaccount.google.com/permissions → Mimbar → "Ondoa ufikiaji". Masomo yaliyokwishachapishwa yanabaki YouTube; Mimbar haitaweza tena kupakia mapya hadi uunganishe tena.
Ukiona "Muunganisho wa YouTube haufanyi kazi tena" au somo likishindwa ghafla baada ya wiki moja hivi — ruhusa imeisha muda wake upande wa Google. Nenda Mipangilio na ubonyeze "Badilisha chaneli" kuunganisha upya. Masomo yako hayapotei.
Hatua 3
Pakia somo
Bonyeza "Pakia somo". Chagua "Sauti tu" (Mimbar itabadilisha kuwa video yenye picha ya jalada) au "Video kamili" (itapakiwa jinsi ilivyo). Weka faili.
Kisha jaza fomu. Vitu vilivyo na "hiari" unaweza kuviruka:
- Kichwa cha somo — hiki ndicho kitakachoonekana YouTube. Mfano: "Darsa ya Fiqh — Somo la 14".
- Aina ya somo — Jumuaa Khutba, Darsa, Tafsiri, Aqida, Sira ya Nabii, Nyingine. Wasikilizaji huchuja kwa aina hii.
- Mzungumzaji — sheikh anayefundisha. Kwa akaunti ya msikiti unaweza kuandika jina la mgeni.
- Jina la mfululizo na kipindi (hiari) — ukiandika "Darsa ya Fiqh" na "Somo la 14" kwenye kila somo, Mimbar inayapanga kama mfululizo mmoja.
- Maelezo na maneno ya utafutaji (hiari) — huongezwa kwenye maelezo ya YouTube. Unaweza kuweka chaguo-msingi Mipangilio ili usiandike kila mara.
- Hali ya faragha — Hadharani (kila mtu), Kwa kiungo tu (aliye na kiungo tu), au Binafsi. Masomo ya Mimbar huonekana kwa umma tu yakiwa Hadharani.
- Ratiba (hiari) — chagua tarehe na saa. Video hupakiwa mara moja kama ya siri, na YouTube huifungua yenyewe saa iliyofika. Hadi wakati huo somo huonekana kwenye ukurasa wa mwanzo wa Mimbar chini ya "Masomo yanayokuja", bila kiungo.
Mara ya pili na kuendelea ni haraka zaidi: Mimbar hukumbuka aina ya picha ya jalada, hali ya faragha na aina ya somo uliyochagua. Utahitaji faili na kichwa tu.
Hatua 4
Chagua picha ya jalada
Picha ya jalada ndiyo picha ndogo inayoonekana YouTube kabla mtu hajabonyeza. Mimbar inaitengeneza kwa ajili yako. Kuna njia sita — tano kati yake hazina picha ya mtu yeyote:
- Maandishi na Michoro — Kichwa cha somo juu ya michoro ya Kiislamu — hakuna picha ya mtu.
- Msikiti na Majengo — Kichwa juu ya picha ya msikiti au mihrab — hakuna picha ya mtu.
- Logo ya Kituo — Logo yako na maandishi tu — chaguo lenye uangalifu zaidi.
- Picha Yangu ya Jalada — Pakia picha ya jalada uliyoitengeneza mwenyewe. (JPG au PNG, hadi 2MB.)
- Acha YouTube Ichague — Hakuna thumbnail maalum; YouTube itachagua fremu. (Video tu)
- Picha ya Mzungumzaji — Picha ya sheikh pamoja na mandharinyuma. Utaweka picha ya sheikh; Mimbar inaondoa mandhari ya nyuma na kuweka mandhari mpya. Unachagua picha ikae kulia, kushoto, katikati au ijaze jalada lote.
Kwa njia zinazotengeneza mandhari, unaweza kuandika unachotaka kuona (mfano: "mihrab ya zamani, mwanga wa dhahabu ukiingia dirishani") au kutumia mandhari uliyotumia mara ya mwisho ili masomo yako yafanane.
Kama hutaki picha ya mtu kabisa: chagua Maandishi na Michoro, Msikiti na Majengo au Logo ya Kituo mara moja Mipangilio kama chaguo-msingi, na hutaulizwa tena. Njia hizi haziwahi kuhusisha picha ya kiumbe hai katika hatua yoyote.
Hupendi picha iliyotoka? Bonyeza "Tengeneza upya" — hadi mara 5 kwa somo moja — au badilisha maelezo ya mandhari na ujaribu tena.
Hatua 5
Thibitisha na chapisha
Hii ndiyo hatua watu husahau. Kuweka faili HAKUCHAPISHI somo. Baada ya picha ya jalada kutengenezwa, lazima uikague na ubonyeze "Thibitisha na anza uchapishaji". Bila hapo somo linakaa kwenye dashibodi yako likisema "Thibitisha picha ya jalada" na haliendi popote.
Ukithibitisha, somo linaingia kwenye foleni na unaweza kufunga ukurasa. Fuatilia hali yake dashibodini:
- Inasubiri picha ya jalada / AI Inatengeneza... — jalada linatengenezwa.
- Thibitisha picha ya jalada — inakusubiri WEWE. Bonyeza "Thibitisha".
- Imeidhinishwa → Inabadilisha Sauti→Video → Inapakia YouTube — Mimbar inafanya kazi. Somo la saa moja huchukua dakika chache hadi kadhaa, kutegemea mtandao.
- Imechapishwa — lipo YouTube. Utapata barua pepe yenye kiungo.
- Imepangwa — lipo YouTube kama la siri; litafunguka lenyewe saa uliyochagua.
- Imeshindwa — kuna hitilafu. Dashibodi inakuonyesha sababu na kitufe "Jaribu tena". Soma "Maswali ya kawaida" hapa chini.
Ukiacha somo katikati — mfano simu ikazima — dashibodi inalionyesha na kitufe "Endelea" au "Thibitisha". Halipotei.
Mipaka na michango
Kupakia ni bure na hakuna kikomo cha masomo kwa mwezi. Msimamizi anaweza kuweka kikomo kwa akaunti moja ikibidi; ukiwekewa, ukurasa wa kupakia utakuonyesha "Mwezi huu: 3 / 10" na sababu.
Ukubwa wa faili: sauti hadi 500MB, video hadi 4GB (kikomo cha YouTube), picha ya jalada hadi 2MB.
Mimbar huendeshwa kwa michango — ya mtu binafsi au ya msikiti — kupitia M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money, kadi ya benki au kadi ya kimataifa. Mchango haununui masomo zaidi wala nafasi ya juu; kila mtu anapata huduma ile ile. Ukitaka kuchangia, tafuta "Changia Mimbar" kwenye menyu.
Maswali ya kawaida
Somo langu linasema "Imeshindwa" na "Video hii ni ndefu kuliko dakika 15, na chaneli yako haijathibitishwa". Nifanye nini?
Chaneli za YouTube ambazo hazijathibitishwa kwa simu hukubali video za hadi dakika 15 tu. Nenda youtube.com/verify ukiwa umeingia kwa akaunti ya chaneli, weka namba ya simu, ingiza msimbo. Kisha rudi dashibodini na ubonyeze "Jaribu tena" — hutahitaji kupakia faili upya.
Somo lilishindwa na ujumbe "Muunganisho wa YouTube haufanyi kazi tena". Mbona? Niliunganisha wiki iliyopita.
Ruhusa uliyotoa Google imeisha muda wake — hutokea baada ya siku 7 hivi kwa sasa. Nenda Mipangilio → Chaneli ya YouTube → "Badilisha chaneli" na uunganishe upya (chagua chaneli ile ile). Kisha dashibodini bonyeza "Jaribu tena" kwenye somo lililoshindwa.
Somo langu limekaa siku nzima likisema "Thibitisha picha ya jalada".
Linakusubiri wewe. Fungua dashibodi, bonyeza "Thibitisha" kwenye somo hilo, kagua picha ya jalada na ubonyeze "Thibitisha na anza uchapishaji". Kuweka faili peke yake hakuchapishi.
Nimeingia lakini "Pakia somo" inaniambia akaunti yangu inasubiri ukaguzi.
Msimamizi wa Mimbar bado hajakagua akaunti yako. Hakuna unachotakiwa kufanya — utapata barua pepe ikishakubaliwa. Ukisubiri, unganisha chaneli yako ya YouTube na ukamilishe wasifu wako ili uwe tayari. Ikipita muda mrefu bila jibu, tuandikie info@himatech.co.tz.
Picha ya jalada imekosea — imeandika kichwa vibaya, au sipendi mandhari.
Kabla ya kuthibitisha: bonyeza "Tengeneza upya" (hadi mara 5) au badilisha njia ya jalada. Baada ya kuchapishwa: picha ya jalada iko YouTube; ibadilishe kutoka YouTube Studio kwenye chaneli yako.
Naweza kufuta somo?
Ndiyo, kama bado halijafika YouTube — rasimu, somo linalosubiri jalada, au lililoshindwa — kwa kitufe "Futa" dashibodini. Somo lililokwishachapishwa au kupangwa LIPO kwenye chaneli yako ya YouTube; Mimbar hailifuti kutoka huko. Lifute kwenye YouTube Studio kwanza, kisha tuandikie info@himatech.co.tz tuliondoe Mimbar.
Faili langu la sauti liko wapi baada ya kuchapishwa?
Mimbar huhifadhi faili lako tu hadi YouTube ilipokee, kisha inalifuta. Picha ya jalada ndiyo inayobaki, kwa ajili ya kuonyesha kwenye tovuti. Video yenyewe iko kwenye chaneli yako.
Naweza kutumia chaneli moja ya YouTube kwa akaunti mbili za Mimbar?
Ndiyo. Akaunti ya msikiti na akaunti ya sheikh zinaweza kuunganisha chaneli ile ile. Kila akaunti inaona masomo iliyopakia yenyewe.
Faragha
Mimbar huhifadhi jina lako, barua pepe, taarifa za wasifu, na taarifa za masomo uliyopakia (kichwa, aina, picha ya jalada, kiungo cha YouTube). Faili la somo hufutwa baada ya YouTube kulipokea. Namba za kadi na simu za malipo hushughulikiwa na watoa huduma wa malipo, si Mimbar.
Ilisasishwa mwisho: 2026-09-20