Ruka hadi kwenye maudhui

Mimbar

Sera ya Faragha

Taarifa gani Mimbar inahifadhi, jinsi inavyotumia taarifa za YouTube, nani mwingine anazipata, na jinsi ya kuziondoa.

Ilisasishwa mwisho: 2026-09-28

Sera hii inahusu nini

Mimbar (mimbar.himatech.co.tz) inaendeshwa na Hima Technology, Zanzibar, Tanzania. Ukurasa huu unaeleza taarifa gani tunazohifadhi unapotumia Mimbar, kwa nini, nani mwingine anazipata, na jinsi ya kuziondoa.

Tumeandika kwa lugha ya kawaida kwa makusudi. Ukiwa na swali lolote, tuandikie info@himatech.co.tz.

Taarifa tunazohifadhi

Ukifungua akaunti ya mchapishaji (Sheikh au Msikiti):

  • Jina, barua pepe na nywila (nywila huhifadhiwa kwa njia isiyosomeka — hatuwezi kuiona).
  • Aina ya akaunti, jina la msikiti, cheo, na picha ya wasifu ukiweka.
  • Chaguo-msingi zako za kupakia: aina ya picha ya jalada, hali ya faragha, lugha, maelezo na maneno ya utafutaji.
  • Hali ya ukaguzi wa akaunti yako, na tarehe ya kukubaliwa.

Kwa kila somo unalopakia:

  • Kichwa, aina, jina la mzungumzaji, mfululizo, maelezo, maneno ya utafutaji, hali ya faragha na ratiba.
  • Picha ya jalada iliyotengenezwa, na picha ya mzungumzaji uliyoweka (kama ulichagua njia hiyo).
  • Kitambulisho cha video YouTube baada ya kuchapishwa, na idadi ya watazamaji tunayosoma kutoka YouTube ili kukuonyesha dashibodini.
  • Faili la sauti au video LENYEWE huhifadhiwa kwa muda tu — hadi YouTube ilipokee — kisha hufutwa kwenye seva zetu.

Ukichangia: kiasi, sarafu, njia ya malipo, namba ya kumbukumbu ya mtoa huduma wa malipo, na namba ya simu kama ulilipa kwa simu. Namba za kadi HAZIPITI Mimbar kamwe — zinashughulikiwa na Pesapal au Stripe moja kwa moja.

Kumbukumbu za usimamizi: msimamizi anapokagua, kukubali, kukataa au kubadilisha akaunti, kitendo hicho huandikwa pamoja na barua pepe ya msimamizi. Hii ni ili maamuzi yaweze kupitiwa.

Ukitembelea tovuti bila akaunti (kama msikilizaji), hatuhifadhi taarifa zako binafsi. Hatutumii vidakuzi vya ufuatiliaji wa matangazo wala huduma za takwimu za nje.

Jinsi tunavyotumia taarifa za YouTube

Mimbar hutumia huduma za YouTube API. Unapounganisha chaneli yako, Google inakuuliza ruhusa ya "kusimamia akaunti yako ya YouTube". Mimbar inaitumia kwa mambo haya tu:

  • Kupakia video za masomo UNAYOWEKA, na kuziwekea kichwa, maelezo, picha ya jalada, hali ya faragha na ratiba uliyochagua.
  • Kusoma jina na kitambulisho cha chaneli, na kama chaneli imethibitishwa (ili kukuonya kabla ya kupakia somo refu kuliko dakika 15).
  • Kusoma idadi ya watazamaji wa video ambazo Mimbar yenyewe ilipakia.
  • Somo likiwa sehemu ya mfululizo: kusoma majina ya orodha zako za kucheza (playlists) ili kupata ya mfululizo huo, kuiunda kama haipo, na kuongeza somo ndani yake.

Mimbar HAISOMI wala kuhifadhi: maoni, wafuasi, historia yako ya kutazama, wala video ambazo haikupakia. Kutoka kwenye orodha za kucheza inasoma majina tu, kama ilivyoelezwa hapo juu, na haihifadhi. Haipakii, haibadilishi wala kufuta chochote bila wewe kubonyeza kitufe cha kuthibitisha.

Tunachohifadhi kutoka YouTube: kitambulisho na jina la chaneli, hali ya uthibitisho, na ufunguo wa ruhusa (refresh token) unaoiruhusu Mimbar kupakia kwa niaba yako. Ufunguo huu hauonyeshwi kwa mtu yeyote, hautumiki kwa jambo lingine lolote, na hufutwa unapotenganisha chaneli.

Jinsi ya kuondoa ruhusa: Mipangilio → Chaneli ya YouTube → "Tenganisha chaneli"; au kutoka Google moja kwa moja kwenye myaccount.google.com/permissions. Masomo yaliyokwishachapishwa yanabaki kwenye chaneli yako.

Matumizi ya Mimbar ya taarifa zinazopatikana kupitia Google API yanafuata Google API Services User Data Policy, ikiwa ni pamoja na masharti ya Limited Use. Kwa kuunganisha chaneli yako unakubali pia Sera ya Faragha ya Google (policies.google.com/privacy) na Masharti ya Huduma ya YouTube (youtube.com/t/terms).

Nani mwingine anapata taarifa

Hatuuzi taarifa zako kwa yeyote. Huduma zifuatazo hupokea sehemu ya taarifa ili Mimbar ifanye kazi:

  • Google / YouTube — video, kichwa, maelezo na picha ya jalada ya kila somo unalochapisha.
  • Huduma za AI za picha (mfano remove.bg kwa kuondoa mandhari ya nyuma ya picha ya mzungumzaji; Stability AI, Google Gemini, OpenAI au nyingine kwa kutengeneza mandhari mpya) — hupokea picha ya mzungumzaji ukichagua njia hiyo, na maelezo ya mandhari unayoandika. Njia zisizo na picha ya mtu hazitumi picha ya mtu yeyote.
  • Cloudinary — hifadhi ya picha za jalada na picha za wasifu (na faili za masomo kwa muda, mpangilio ukiwekwa hivyo).
  • Pesapal na Stripe — malipo ya michango. Wanapokea kiasi, barua pepe na (kwa malipo ya simu) namba ya simu.
  • Mtoa huduma wa barua pepe — anwani yako na maudhui ya barua tunazokutumia (somo limechapishwa, hitilafu, uamuzi wa ukaguzi).
  • Mwenyeji wa seva zetu, ambako data huhifadhiwa.

Kila mmoja wao ana sera yake ya faragha na anapokea taarifa zinazohitajika kwa kazi yake tu.

Kinachoonekana hadharani

Ukiwa mchapishaji aliyekubaliwa, mambo haya huonekana kwenye tovuti kwa kila mtu: jina lako au la msikiti, cheo, picha ya wasifu, jina la chaneli ya YouTube, na masomo uliyochapisha kama "Hadharani" (kichwa, aina, picha ya jalada, mzungumzaji, idadi ya watazamaji). Barua pepe yako haionyeshwi kamwe.

Masomo uliyoweka "Kwa kiungo tu" au "Binafsi" hayaorodheshwi kwenye tovuti. Akaunti ambayo haijakubaliwa au imekataliwa haionekani kwenye tovuti kabisa.

Barua pepe tunazotuma

Tunakutumia barua pepe pale tu inapohusu akaunti yako: ukifungua akaunti, uamuzi wa ukaguzi, somo likichapishwa, au likishindwa. Hatutumi barua za matangazo.

Kufuta taarifa zako

Unaweza kufuta rasimu na masomo ambayo hayajafika YouTube wewe mwenyewe kutoka dashibodini. Kufuta akaunti nzima: tuandikie info@himatech.co.tz kutoka barua pepe ya akaunti, na tutaifuta ndani ya siku 7 pamoja na masomo yake yote kwenye Mimbar. Video zilizoko kwenye chaneli yako ya YouTube ni zako; Mimbar haizifuti kutoka huko.

Kutenganisha chaneli ya YouTube (Mipangilio) hufuta ufunguo wa ruhusa mara moja.

Usalama

Muunganisho wote ni kwa HTTPS. Nywila huhifadhiwa kwa njia isiyosomeka (bcrypt). Funguo za ruhusa za YouTube hazionyeshwi kwenye kiolesura chochote. Wasimamizi wanaoweza kuona taarifa za akaunti ni wachache, na kila kitendo chao huandikwa.

Mabadiliko ya sera hii

Tukibadilisha sera hii, tarehe iliyo chini ya ukurasa itabadilika. Mabadiliko makubwa tutayatangaza kwa barua pepe kwa wachapishaji.

Mawasiliano: info@himatech.co.tz · +255 628 404 865 · Hima Technology, Zanzibar, Tanzania.